Search This Blog

November 8, 2012

JE WAWAJUA MAWAZIRI WENYE MVUTO KUPITA WENGINE BONGO???TANZANITE GLAMOUR NAMU ENDORSE MAGUFULI WAKIFUATIWA NA WOTE WALIOTAJWA!!!!


Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wametajwa kuwa na mvuto kwa mwaka 2012 kutokana na utendaji kazi wao uliotukuka.
Wafuatao ni mawaziri 10 waliotajwa na baadhi ya Wabongo waliozungumza na Amani juzikati:

Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison George Mwakyembe:
Anatajwa kuongoza kwa mvuto kutokana na juhudi zake za kufufua Shirika la Reli Tanzania na kufanikisha utumikaji wa treni jijini Dar es Salaam. Pia anasifiwa kwa jinsi anavyowapiga chini viongozi wabadhirifu wa mali za umma.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli:
Yeye amepewa ujemedari kwa kusimamia barabara nchini na amekuwa akivutia kwa jinsi anavyohakikisha barabara zote kuu zinapitika kwa kiwango cha lami (japokuwa barabara ya Kibiti-Lindi inalalamikiwa sana).

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka:
Amekuwa na mvuto kutokana na sera yake ya kuwanyang’anya viwanja wale wote waliojinufaisha na maeneo ya wazi na waliojenga ufukweni kinyume cha sheria. Pia kujenga nyumba kupitia NHC na kuziuza kwa gharama nafuu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki:
Yeye ana sifa kuu moja. Kuwang’oa watendaji katika wizara yake ambao miaka ya nyuma walishindikana licha ya kukabiliwa na tuhuma nzito za ubadhirifu wa mali asili za nchi.


Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo:
Huyu bwana ameuvutia umma kwa kusimamia vyema madini na hasa nishati ya umeme. Kuingia kwake kwenye wizara hiyo kumesababisha kung’olewa kwa viongozi kadhaa waliokuwa na tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya kazi akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Tanesco, William Mhando.
Aidha, amependwa kwa kutangaza kwake kwamba, nchi haitakuwa na mgao wa umeme kama zamani.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel John Sitta:
Amekuwa na mvuto kutokana na kujipambanua kuwa ni mpiganaji vita dhidi ya wala rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kwingineko.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Ally Hassan Mwinyi:
Amekuwa na mvuto kwa sababu ya kusimamia huduma za afya na hasa kwa upande wa madaktari. Tangu kuchaguliwa kuongoza wizara hiyo kuna maelewano kati ya serikali na madaktari.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene:
Yeye licha ya kuwa msaidizi wa waziri, amekuwa kivutio kwa jinsi anavyomsaidia waziri Muhongo kuongoza vyema wizara hiyo ndani na nje ya bunge.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo A. Mulugo:
Huyu jamaa haogopi mtu bwana, amekuwa kivutio kwa kuwa ni mwiba mkali kwa walimu wazembe na watumishi mbalimbali wa wizara ya elimu nchini licha ya juzikati kuchanganya ‘madawa’ huko Afrika Kusini kwa kutamka visivyo nchi zilizounganishwa na kuwa Tanzania.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Samuel Nyalandu:
Amekuwa na mvuto kutokana na kushirikiana vyema na Waziri Kagasheki katika kusimamia utalii na maliasili hadi kutegemea kuingizia nchi fedha nyingi za kigeni

No comments:

Post a Comment

ABUSIVE LANGUAGE IS NOT ALLOWED TO THIS BLOG. THANK U FOR UR COOPERATION

Note: Only a member of this blog may post a comment.

YOU MAY ALSO LIKE THIS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...