Search This Blog

November 13, 2012

BONGO UNYAMA UNYAMA: MWANAMKE AUAWA KWA RISASI AKIPANDA DALADALA


Na Makongoro Oging'
Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Veronica Masai (29) (pichani) mkazi wa Manzese, jijini Dar es Salaam ameuawa kwa kupigwa risasi mbele ya mumewe wakati wakipanda daladala katika kituo cha Davis Corner, wilaya ya Temeke hivi karibuni.
Habari zilizopatikana eneo la tukio zinaeleza kwamba Veronica aliuawa kwa risasi na mtu anayesemekana anajulikana na mauaji hayo yalifanyika mbele ya mumewe aitwaye Athumani Masai (41) ambaye pia alipigwa risasi mkononi na bega la kulia.
Taarifa zilizopatikana kwa mume wa Veronica zinadai kwamba marehemu wakati anapigwa risasi alikuwa amembeba mtoto wake wa umri wa miezi nane wakitoka katika shughuli zao za biashara, Abiola maeneo ya Yombo.
Athumani alimsimulia mwandishi wetu mkasa mzima kama ifuatavyo: “ Siku ya tukio nakumbuka ilikuwa saa 3.30 usiku wakati nikimpisha mke wangu mlangoni ili apande daladala lililokuwa likielekea Kariakoo ambapo tulitegemea kupata usafiri mwingine kwa urahisi hadi Manzese tunakoishi.
“Nikiwa nimeshikilia gari mke wangu alikuwa nyuma yangu, nilipogeuka kumpisha ili atangulie kuingia  akiwa amembeba mtoto ndipo nilipigwa risasi mgongo ikatokea begani na kuvunja mfupa wa kulia.
“Mke wangu alipogeuka nyuma kuangalia ilipotokea risasi, alimuona mtu anayemfahamu, alimuuliza shemeji kwa nini unamuua mume wangu? Ndipo naye alipigwa risasi, alimuachia mtoto akadondoka chini, wote tukawa tupo chini.
“Baada ya watu kusikia mlio wa risasi, walitawanyika nalo daladala lilitoweka, kwa kweli eneo lile lilibaki jeupe, nilibaki na familia yangu tu.
“Mke wangu alikuwa akilia kwa uchungu huku akiomba nimuwahishe hospitali, mwanangu alipoteza fahamu.
“Niliwaona watu wawili wakiwa wamepanda pikipiki,  mmoja alifyatua risasi hewani, naamini ndiyo waliotushambulia, walikua wakitoroka wakijua wameshatumaliza. “Nipoteza fahamu na baada ya kuzinduka nilijikuta nipo Hospitali ya Temeke kisha nikahamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na siku ya pili yake niliambiwa mke wangu amefariki, niliumia sana. Mazishi yalifanyika Karatu na wala sikupata nafasi ya kuuaga mwili wake.
“Nilipata nafuu mwezi wa sita mwaka huu na sasa najiandaa kwenda kuona alipozikwa mke wangu japokuwa wabaya wangu bado wananitumia meseji za vitisho na polisi hawafuatilii japokuwa wamefungua jalada lenye kumbukumbu namba CHA\RB\9423\2011 katika Kituo cha Chang’ombe,” alisema Athumani.

No comments:

Post a Comment

ABUSIVE LANGUAGE IS NOT ALLOWED TO THIS BLOG. THANK U FOR UR COOPERATION

Note: Only a member of this blog may post a comment.

YOU MAY ALSO LIKE THIS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...