Search This Blog

July 16, 2012

YALIYOCHUKUA NAFASI MAGAZETINI JANA NIMECHAGUA YALIYONIGUSA!!!!!

Na Khatimu Naheka
HATIMAYE wanachama wa Yanga kwa moyo mmoja usiku wa kuamkia leo walimchagua mfadhili wao wa zamani, Yusuf Manji kuwa mwenyekiti wa timu hiyo, lakini majira ya saa nane usiku kabla hajatangazwa zilizuka vurugu kubwa.
Yanga jana ilifanya uchaguzi wa kujaza nafasi kadhaa ambazo ziliachwa wazi baada ya mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Llyod Nchunga, makamu mwenyekiti, Davies Mosha na wajumbe kadhaa kujiuzulu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar, zaidi ya wanachama 2,000 walipiga kura, huku amani ikitawala kuanzia hatua za awali, lakini hali mbaya ilizuka usiku majira ya saa nane baada ya walinzi kujisahau na kufungua geti wakifikiri kuwa kura zimemalizika kuhesabiwa, ndipo mamia ya wanachama waliokuwa nje ya ukumbi huo kuingia ndani kwa kasi.
Hata hivyo, wasimamizi waliwataka wanachama hao kutoka nje kwanza kwani kura za mwenyenyekiti zilikuwa bado hazijahesabiwa, hali iliyozua zogo na kejeli za hapa na pale.
“Nyie vipi sisi tumekaa hapa kuanzia asubuhi halafu saa hivi mnatuambia kuwa bado hamjamaliza, mbona miaka mingine tunakuwa zaidi ya wanachama 3,000 na tunamaliza mapema nyie…….. (anatukana) msitufanye sisi watoto wadogo,” alisema mwanachama mmoja.
Hali hiyo, iliwalazimu walinzi kufanya kazi yao ambapo waliwalazimisha wanachama hao kutoka nje hali iliyozua vurugu kubwa.
Picha halisi ya Manji kushinda kwa kishindo ilionekana mapema kabisa hata kabla wanachama hao hawajaanza kupiga kura zao.
Wakati akiingia ukumbini hapo akiwa na wapambe wake, wanachama wote walisimama na kushangilia kwa nguvu zote hali iliyoonyesha kuwa alikuwa na nafasi kubwa ya kupata kura nyingi zaidi ya wagombea wengine, Joel Jembele na Edgar Chibura.
“Ukweli ni kwamba mpaka sasa Manji anaongoza kwa kura nyingi sana. Kila tukihesabu kura sabini ndiyo tunapata mtu mwingine kwa hiyo atashinda kwa asilimia kubwa sana,” kilisema chanzo cha ndani kilichokuwa kinahusika kuhesabu kura hizo majira ya saa nane na dakika 26 usiku.
Mbali na mwenyekiti na makamu, hali inaonyesha kuwa timu kamili ya Manji iliiingia kwenye uongozi huo baada ya Abdallah bin Kleb pamoja na Mussa Katabalo waliokuwa wakigombea nafasi ya ujumbe wa kamati kuu habari za ndani kusema kuwa wametwaa nafasi hiyo.
Moja ya mambo ambayo uongozi huo mpya unaweza kufanya ni kuhakikisha timu hiyo inakuwa na uwanja wa kisasa, kitu ambacho kimekuwa kikipigiwa kelele na mwenyekiti huyo mara kwa mara.

SOURCE: GP

No comments:

Post a Comment

ABUSIVE LANGUAGE IS NOT ALLOWED TO THIS BLOG. THANK U FOR UR COOPERATION

Note: Only a member of this blog may post a comment.

YOU MAY ALSO LIKE THIS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...