Search This Blog

April 26, 2012

Watanzania watakufa wakiujadili Muungano?......Tanzania Daima.

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na upungufu wake inatoa uhuru wa mawazo kwa kila mtu, katika ibara ya 18(a).
Hivyo pasi ajizi kutoka kwenye sakafu ya mtima wangu, napenda kutumia ibara hiyo kueleza fikra zangu juu ya Tume ya Katiba iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kitabu kitakatifu cha Biblia kinatanabaisha kwamba: “Bwana Mungu akamtoa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Eden, ailime na kuitunza, Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu akisema, matunda ya kila mti wa bustani waweza kula walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”
Hapa Mungu anampa Adam maelekezo na masharti yote ili asile tunda la mti wa katikati, kwani akila anaweza kufa.
Kwa upande wa Tanzania hii yenye neema badala ya kutoa maziwa na asali, inatoa ndimu na pilipili kwa watu wake.
Imeteuliwa tume iwanyamazishe Watanzania wote watakaozungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ni kwanini rais anazuia? Je, Muungano ni eneo la mema na mabaya kama ilivyo mti wa elimu ya mema na mabaya kule Eden, kwamba Watanzania wakihoji watakufa?
Je, rais wetu anajua kuwa anawazuia waliomchagua 2010 pia? Kwa wale wasiofahamu, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika siku ya Jumapili, Aprili 26 1964. Wakati huo Kikwete alikuwa na miaka 14 tu.
Rais anaweza asihoji Muungano kwa sababu alikuwapo. Je, waliozaliwa Aprili 27, 1964 hawana haki ya kuhoji Muungano?
Nadhani wanayo haki ya kuhoji kuhusu Muungano ili waufahamu ukoje, ulikuwaje na kadhalika.
Rais anatakiwa aache hofu, awaache Watanzania wajadili Muungano, waamue wanataka Muugano wa aina gani na si awaamulie aina ya Muungano wanaohitaji.
Labda rais atueleze Watanzania tutakufa kama tukiujadili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ukizingatia Mungu alimwambia Adam akila tunda la mti wa katikati ya bustani wenye ujuzi wa mema na mabaya atakufa.
Watanzania wasipokonywe haki yao ya kujadili mambo wanayoyahitaji, Rais wetu akumbuke kwamba, mtu anaweza kumbembeleza mtoto mdogo anayelia kwa kumnunulia pipi na akanyamaza, ila ni vigumu kumbembeleza mtu mzima anayelia kwa kunyang’anywa haki yake kwa kumnunulia pipi.
Atafakari na aachie uhuru wa kujadili masuala nyeti ya nchi hii, kwa nini rais aiagize Tume ya Katiba ikusanye maoni yote ila ya Muungano wa namna gani hapana?
Kwanini Watanzania wazuiwe kujadili mustakabali wa nchi yao? Kwa misingi hiyo hapakuwa na haja ya kuundwa kwa Tume ya Katiba inayoongozwa na gwiji, Joseph Sinde Warioba.
Taifa letu lina nusu karne tangu lilipopata Uhuru saa sita kamili usiku, siku ya Jumapili, Desemba 9, 1961 kutoka kwa Waingereza kufuatia jitihada za hayati Mwalimu Nyerere, hivyo tunahitaji katiba itakayodumu zaidi ya miaka 1,000.
Katiba itakayotungwa ikiacha mawanda mapana ya majadiliano, Watanzania watakuwa na umiliki na katiba hiyo. Kuna baadhi ya wanaamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una matatizo na si changamoto.
Hivyo ni wakati mwafaka kwa, wananchi wa pande zote za muungano wajadili kwa uhuru, watoe mawazo yao ili mradi yasiwe matusi.
Rais akumbuke kuwa kuchunguza tatizo kunaweza kufananishwa na kipindi cha miezi ya ujauzito, na kulitatua tatizo ni sawa na siku ya kuzaliwa mtoto huyo, kwa hakika maana halisi ya kulichunguza tatizo ni kulitatua.
Hivyo rais awaache wananchi wa pande zote mbili watafute mwarobaini wa tatizo pasi kuwafunga midomo yao.
Tukiangalia picha iliyopigwa Aprili 26, 1964 wakati wa kuundwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nyerere anaonekana ameshika vibuyu viwili vyenye udongo akichanganya udongo wa Zanzibar na Tanganyika ila Rais Abeid Aman Karume yupo pembeni kidogo akiwa anashangaa!
Maswali! ni kwa nini Mwalimu hakushika kibuyu kimoja chenye udongo wa Tanganyika na mzee Abeid akashika kibuyu chenye udongo wa Zanzibar halafu wakuu hao wakachanganya kwa pamoja?
Hapa kuna ujumbe mzito mithili ya msitu wa Amazon, na usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Tuyaache hayo kwani ni mazito! Ila tunatakiwa tufikirie nje ya maboksi ili tutanabaishe maktaba ya mwonekano huo wa picha.
Kwa weledi wangu, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu kisiasa, kiuchumi, na kijamii.
Nasisitiza na kushadadia kuwa, kwa yeyote anayepinga Muungano ni sawa na mtu anayepinga Muungano wa baba yake na mama yake ambapo yeye ni zao la Muungano huo, kwa tasfiri pana maana yake anajipinga mwenyewe hata baba na mama wakitengana huwezi kurudi tena tumboni kwa mama yako, au kurudi kwenye mfumo wa uzazi wa baba yako, utabaki kuwa zao la muungano wa baba na mama.
Hivyo Watanzania kwa pamoja tuujadili Muungano kwa pamoja, tukubaliane kwa pamoja. Kwani yatupasa tupingane pasi kupigana, tukosoane pasi kukoseana, tuwajibishane pasi kuaibishana wakati tunatoa maoni yetu juu ya katiba tuitakayo.
Inafahamika wazi kuwa Watanzania wa leo wana ufahamu tambuzi, wana weledi akinifu juu ya masuala nyeti ya nchi hii.
Mathalani, Tanganyika ilipata Uhuru Desemba 9 1961, ikaungana na Zanzibar mnamo siku ya Jumapili mchana Aprili 26, 1964 na kupata Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ila tunasherehekea kila mwaka sikukuu ya kuzaliwa Tanganyika na cha ajabu mwaka 2011 zaidi ya sh bilioni 60 za Kitanzania ziliteketezwa kwa ajili ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika.
Kwa maneno mengine bado Tanganyika ipo, kama ilikuwa haipo, tusinge sherehekea Desemba 9, kila mwaka bali Aprili 26, kila mwaka. Sina maana kuwa nina mawazo ya kuvunja Muungano, kuibua hii hoja kuna maanisha bado mambo hayapo sawa, lazima wananchi wa pande zote mbili wajadili kuhusiana na Muungano. Tujue tunataka muungano wa namna gani.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18(a) imeshavunjwa kwa wananchi kunyimwa haki wasijadili kuhusu suala nyeti la Muungano wa namna gani unatakiwa.
Cha ajabu katiba hiyohiyo ibara ya 46(1) (2) inamruhusu rais aendelee kuvunja katiba kwani hakuna yeyote anayeweza kumfungulia mashitaka wakati akiwa pale Ocean Road (Ikulu).
Rais wetu aliyechaguliwa na Watanzania takriban milioni tano kati ya milioni 20 waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2010, tunamwomba awape uhuru Watanzania wote pamoja na wale wenye miaka 14, hata wenye miaka mitano ilimradi wawe wanajua kuongea ili waweze kujadili kinagaubaga kuhusu suala la Muungano ili mwishowe mawazo yetu sote yawe yanaelea katika dimbwi moja la mwafaka wa kitaifa.
Watanzania wasipewe masharti kama Mungu alivyompa Adam kuhusu tunda la mti wa katikati kwamba angekula angejua mema na mabaya.
Hivyo tuachiwe tule tunda la Muungano ili tujue mema na mabaya yake kwa ajili ya mustakabali wetu, wajukuu, vitukuu, vining’ina, vilembwe na vilembwekeze vyetu.
Tukiona mabaya baada ya kujadili tunda letu la muungano tutatue, tukiona mazuri tuyaendeleze kwa utashi mwema.
Binadamu wote si sawa, na si wakamilifu, mimi ni binadamu, kwa hiyo mimi si sawa na mkamilifu, kama nimekosea katika makala hii tusamehane, turekibishane ili tuijenge Tanzania tunayoiota, ili miaka 50 ijayo tuikopeshe Marekani.
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Afrika Mashariki, Mungu ibariki Tanzania yetu.0784- 423458/ 0712830357 jejulius@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ABUSIVE LANGUAGE IS NOT ALLOWED TO THIS BLOG. THANK U FOR UR COOPERATION

Note: Only a member of this blog may post a comment.

YOU MAY ALSO LIKE THIS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...