MWENYEKITI Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, anatarajiwa kutunukiwa tuzo mbili za kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Global 2000(2010), Dk. William Morris, alizitaja tuzo hizo kuwa ni pamoja na ile ya kimataifa ya Uongozi na Ubinadamu na Tuzo ya kimataifa ya mafanikio katika maisha, na zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Dk. Mengi katika halfa itakayofanyika Aprili 28 katika ukumbi wa Hoteli ya Serena.
“Dk. Mengi ni Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya Umoja wa Mataifa, ambayo hutolewa kwa watu waliojitolea maisha yao kuleta maendeleo, kusaidia vikundi na watu mbalimbali, amefanya mambo mengi ya kustaajabisha,” alisema Dk. Morris.
Mengi amefanikiwa kushinda kutokana na kujitoa katika masuala hayo pamoja na kufanikisha harakati za kupambana na vita dhidi ya umaskini, ufisadi, elimu, magonjwa, njaa na mambo mengine mengi.
Tuzo hiyo hutolewa mara moja kwa mwaka na Baraza la Umoja wa Mataifa na wameitoa kwa Dk. Mengi baada ya kuibuka kinara miongoni mwa majina 10,000 yaliyopendekezwa ambapo majina matatu ya mwisho, hupigiwa kura na Baraza la Umoja wa Mataifa kupitia mashirika na taasisi za umoja huo.
Alisema jina la Dk. Mengi lilipendekezwa tangu mwaka 2008, 2009, lakini hakuchaguliwa.
“Mwaka 2010 jina lake liliingizwa tena, tukaanza kufuatilia shughuli zake na mambo aliyofanya kwenye jamii, hakutukuamini, tumekusanya mikanda ya video yote ya shughuli alizofanya, hakika tumeshangazwa na mtu wa aina yake na safari hii alipigiwa kura ya ushindi wa asalimia 80,” alisema Dk. Morris.
Tuzo hiyo ilizinduliwa mwaka 2007 na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na kusajiliwa rasmi katika Idara ya Mawasiliano ya Umma (DPI-NGO) na Baraza la Uchumi na Jamii ya Umoja wa Mataifa.
SOURCE: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment
ABUSIVE LANGUAGE IS NOT ALLOWED TO THIS BLOG. THANK U FOR UR COOPERATION
Note: Only a member of this blog may post a comment.