Stori: Haruni Sanchawa na George Kayala
VYOVYOTE vile inaweza kuzungumzwa lakini ukweli utasimama kuwa mtoto Gift Mustapha, 4, hakustahili kuuawa.
Mwili wa marehemu Gift Mustapha ukipelekwa kuzikwa.
Gift, pamoja na umri wake mdogo, kilichomponza ni uelewa wake, pale alimpomfuata baba yake, Mustapha Mchele, 37, akimhoji sababu ya kumpiga mama yake.
Mtoto Gift Mustapha enzi za uhai wake.
Ni mtoto mdogo lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo ndiyo maana alipowakuta baba na mama yake wanapigana, haraka sana alihoji sababu ya ugomvi wao, akataka waachiane.
Kumbe baba ni katili, eti swali “kwa nini baba unampiga mama”, likamuudhi, hivyo akamcharanga mapanga Gift mpaka akapoteza maisha.
Mtoto Gift, ameuawa kikatili mno, picha za tukio tumeshindwa kuzitumia kutokana na maadili, zinaonesha jinsi muuaji alivyomkatakata usoni na kichwa kizima bila huruma.
Gift, aliuawa Desemba 10, 2012, nyumbani kwao, Yombo Buza, Temeke, Dar es Salaam.
Mama wa marehemu, Zulfa Mustapha na majirani zake, wanamlilia Gift, wakimuelezea alikuwa mtoto mzuri, mwenye akili na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo licha ya umri mdogo aliokuwa nao.
SIKU YA TUKIO
Jirani aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema, Gift alikuwa anatoka madrasa, alipofika nyumbani aliwakuta wazazi wake wanagombana.
“Ni kawaida ya Gift kufuatawa na ama baba yake au mama yake pindi anapokuwa madrasa lakini siku hiyo hakufuatwa, kwa hiyo alifika nyumbani amechelewa kidogo.
“Inaonekana alisubiri kwa muda kabla ya kuamua kurudi mwenyewe. Akakuta wazazi wake wanagombana, hakujua kama amekikaribia kifo chake.
Baba wa marehemu ambaye ndiye mtuhumiwa, Mustapha Mchele (37).
“Mama yake alikuwa analia, kwa hiyo akamuuliza baba yake ni kwa nini alikuwa anampiga mama yake. Hapohapo, baba mtu akachukua panga na kumcharanga.
“Baada ya kumcharanga mtoto, akamgeukia mkewe, akamkata mkononi na kichwani jeraha moja lakini mama mtu yeye alipata upenyo na kukimbia,” alisema jirani huyo.
MAMA ALIPONA
Ripota wetu, walifanikiwa kumuona Zulfa akiwa na majeraha mawili, moja mkononi na lingine kichwani lakini hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Hata hivyo, jitihada za maripota wetu kuzungumza na Zulfa ziligonga mwamba kutokana na ndugu zake kuwa wakali.
Wikiendi iliyopita, maripota wetu walifika nyumbani kwake lakini wakaelezwa kwamba ndugu zake wamemhamishia sehemu nyingine.
MTOTO AZIKWA
Gift, alizikwa Desemba 12, mwaka huu kwenye makaburi ya Yombo Buza, Temeke, Dar es Salaam.
Simanzi ilitanda kwa wakazi wa Yombo, husasan majirani wa familia ya Mustafa Mchele, kwani tukio hilo limekuwa na sura ya aina yake.
Mama mzazi wa marehemu Gift Mustapha.
KUHUSU MUUAJI
Majirani wamesema kuwa Mustafa hakutegemewa na jamii kutenda mauaji hayo kutokana na asili yake ya upole na ukarimu kwa watu.
Wamesema kuwa pia ni mtu anayemjua Mungu vilivyo, kwani husali swala tano.
“Ni msomi, alikuwa akiishi na familia yake vizuri. Tuliposikia mauaji haya tumeshangaa sana, wengi wamehisi kuna mambo ya uchawi hapa,” alisema jirani huyo na kuongeza:
“Wengi wanaamini akili ya Mustafa imechezewa. Katika siku za hivi karibuni kila alipokuwa akienda kazini alikuwa akiumwa, akirejea nyumbani huwa mzima.”
Waombolezaji wakiwa msibani.
Jirani mwingine ambaye naye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema: “Mustafa alikuwa anafanya kazi kwenye kiwanda kimoja kilichopo Barabara ya Nyerere lakini siku za karibuni, alikuwa nyumbani mara nyingi kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
“Kule kiwandani ni kiongozi wa wafanyakazi. Kwa nini aumwe akiwa kazini, akifika nyumbani anapona? Mbona si mtu wa ugomvi, sasa ilikuaje agombane na mkewe kisha amuue mtoto wake kipenzi? Kuna kitu hapa!”
Majirani walisema, Mustafa alikuwa anampenda mno Gift na hata siku ya tukio aliongozana naye mpaka madrasa ambako mtoto huyo alikuwa anasoma.
Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu.
KWELI KIFO KINAITA
Kwa mujibu wa majirani, Gift alikuwa akiishi kwa baba yake mkubwa Kigamboni, Dar es Salaam.
Imeelezwa kwamba mwezi uliopita, mtuhumiwa huyo alimfuata Gift ili aishi naye, vilevile asome madrasa lakini Desemba 10, 2012, likatokea tukio hilo la kutisha.
Mustafa alikamatwa na polisi na anashikiliwa katika Kituo cha Chang’ombe, Temeke, Dar es Salaam.